DC MONGERA APONGEZA UBUNIFU WA SUA KAMPASI YA MIZENGO PINDA MAADHIMISHO YA WIKI YA NYUKI TABORA

Mkuu wa Wilaya ya Kaliua, Mheshimiwa Gerald Mongera, amekipongeza Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Kampasi ya Mizengo Pinda, kwa kuwa mstari wa mbele katika kuleta mapinduzi ya kiteknolojia kwenye sekta ya ufugaji nyuki nchini kupitia mafunzo ya vitendo na bidhaa bora.

Pongezi hizo amezitoa leo alipotembelea banda la kampasi hiyo katika Maadhimisho ya Wiki ya Nyuki Kitaifa yanayofanyika Mkoani Tabora kwenye Viwanja vya Kumbukumbu ya Vita.

Akiwa bandani hapo, Mheshimiwa Mongera alipokelewa na kupatiwa maelezo ya kina kutoka kwa Carine John Singu, mwanafunzi wa mwaka wa pili anayesoma Shahada ya Awali ya Usimamizi wa Rasilimalinyuki (Bachelor of Science in Bee Resources Management).

Mwanafunzi huyo alimweleza Mkuu wa Wilaya kuhusu kozi za kimkakati zinazotolewa chuoni hapo, pamoja na kuonyesha vifaa vya kisasa vinavyotumika katika kujifunzia, uvunaji, na uchakataji wa asali safi na mazao mengine ya nyuki.

Mh. Mongera alivutiwa na namna chuo kinavyochanganya nadharia na vitendo, hasa kwa kuona mizinga ya kisasa na vifaa vya uchakataji vinavyoandaliwa na wataalamu pamoja na wanafunzi wenyewe kupitia karakana na viwanda vya chuo.

“Hivi ndivyo vyuo vyetu vinatakiwa kufanya. Sio tu kutoa vyeti, bali kutoa wataalamu wenye ujuzi wa vitendo na uwezo wa kubuni vifaa vinavyoenda kutatua changamoto za wafuga nyuki wetu kule vijijini na kuongeza thamani ya asali yetu,” alisema Mh. Mongera.

Kwa upande wake, Carine alibainisha kuwa elimu wanayopata SUA Kampasi ya Mizengo Pinda inalenga kumjenga mwanafunzi kuwa mjasiriamali na mshauri wa masuala ya nyuki, ili akihitimu aweze kujiajiri na kuajiri wengine badala ya kusubiri ajira za serikalini.

Maadhimisho ya Wiki ya Nyuki Kitaifa yanaendelea mkoani Tabora, huku banda la SUA Kampasi ya Mizengo Pinda likiwa kivutio kikubwa kwa wananchi, wadau wa mazingira, na viongozi mbalimbali wanaotaka kujifunza mbinu za kisasa za ufugaji nyuki wa kibiashara.

Related Posts

SUA KAMPASI YA MIZENGO PINDA YAZITIKISA SHULE ZA SEKONDARI MLELE: YAHAMASISHA TAALUMA NA KUTANGAZA FURSA ZA UDAHILI

Katika juhudi za kuendeleza hamasa ya kielimu na kusogeza huduma za elimu ya juu karibu na jamii, Chuo Kikuu cha...

SUA Kampasi ya Mizengo Pinda Yachochea Ndoto za Wanafunzi Halmashauri ya Mpimbwe kupitia Ziara ya Hamasa.

Katika jitihada za kusogeza elimu ya juu karibu na jamii na kuibua hamasa ya kimasomo, Chuo Kikuu cha Sokoine cha...

Mwenyekiti wa Bodi, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Kampasi ya Mizengo Pinda, Dkt. Zacharia Malley aongoza shughuli ya upandaji miti SUA Kampasi ya Mizengo Pinda

Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Kampasi ya Mizengo Pinda, Dkt. Zacharia Malley, ameongoza shughuli...

Leave a Reply