SUA Kampasi ya Mizengo Pinda Yafanya Vizuri Katika Maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani

Kampasi ya Mizengo Pinda ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) ilishiriki kwa mafanikio katika maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani yaliyofanyika mkoani Dodoma, yakiwa yamefungwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango, tarehe 20 Mei 2024.

 

Dkt. Philip Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alikabidhiwa tuzo na Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki, kama ishara ya kutambua mchango wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kukuza sekta ya ufugaji nyuki na uhifadhi wa mazingira nchini. Tuzo hiyo ilitolewa wakati wa maadhimisho ya kitaifa ya siku ya nyuki yaliyofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete.

 

Katika maadhimisho hayo, Makamu wa Rais Dkt. Mpango alitoa wito kwa wale wote wenye jukumu la kusimamia maeneo yaliyohifadhiwa kuyalinda na kuyaendeleza ili yasiharibiwe na shughuli za kibinadamu. Aidha, aliitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kushirikiana na wadau mbalimbali katika kutoa elimu kwa wafugaji nyuki ili waweze kufuga kwa njia za kisasa kwa kutumia vifaa sahihi, hali itakayoongeza kiwango cha uzalishaji na ufugaji wenye tija.

 

Miongoni mwa wadau waliotajwa na Makamu wa Rais ni pamoja na SUA Kampasi ya Mizengo Pinda, ambayo inatoa Shahada ya Awali ya Sayansi katika Usimamizi wa Rasilimali Nyuki, ikishirikiana na wataalamu kutoka chuo hicho kutoa elimu kwa wafugaji wa nyuki na kuongeza uzalishaji.

 

Mbali na SUA, Makamu wa Rais pia alivitaka Vyuo vya Ufundi Stadi (VETA) vilivyopo katika maeneo yanayofaa kwa ufugaji nyuki kuanzisha kozi zinazohusiana na ufugaji nyuki na uchakataji wa mazao yatokanayo na nyuki.

 

Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki, alisema kuwa Wizara itaendelea kushirikiana na wadau ili kuongeza kasi ya ufugaji nyuki na kuhakikisha kuwa uzalishaji wa asali unaongezeka kutoka tani 32,671 za sasa hadi kufikia lengo la tani 138,000 ifikapo mwaka 2034. Waziri alieleza kuwa Wizara itaongeza uzalishaji wa chavua, kuhamasisha na kuongeza idadi ya mizinga, kuongeza uzalishaji wa asali ya nyuki wasiodunga, na kuongeza thamani ya aina sita za mazao ya nyuki kwa kutumia mazao mengine kama vile sumu ya nyuki na gundi ya nyuki.

 

Waziri Kairuki pia alisema kuwa Wizara itawajengea uwezo wadau na wataalamu ili waweze kufanya kazi kwa ushirikiano zaidi, na kutenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha kuwa vifaa na miundombinu vinaboreshwa katika maeneo ya ufugaji nyuki.

Katika picha ni baadhi ya wadau waliojitokeza katika maadhimisho hayo yaliyofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete mkoani Dodoma, wakitembelea banda la SUA na kupata maelezo kuhusu matumizi ya mashine ya kukamulia asali kutoka kwa Prosper Mahenge, mwanafunzi wa mwaka wa pili anayesoma Shahada ya Awali ya Sayansi ya Usimamizi wa Rasilimali Nyuki katika Kampasi ya Mizengo Pinda iliyopo mkoani Katavi.

Related Posts

Chuo Kikuu Cha Sokoine Cha Kilimo (SUA) na Halmashauri ya Mpimbwe Yaingia Ubia wa Kielimu na Utafiti kwa Maendeleo ya Kilimo

Katika hatua ya kipekee ya kushirikiana kwa maendeleo ya jamii, Chuo Kikuu Cha Sokoine Cha Kilimo (SUA)  kimeungana na Halmashauri...

Uteuzi wa Prof. Jeremia R. Makindara kuwa Kaimu Naibu Rasi wa Ndaki ya Kampasi ya Mizengo Pinda

Uteuzi wa Prof. Jeremia R. Makindara kuwa Kaimu Naibu Rasi wa Ndaki ya Kampasi ya Mizengo Pinda (Utawala na Fedha)